

Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya China yadumisha uhimilivu licha ya changamoto kali za nje
BEIJING - Biashara ya nje ya China imeonyesha unyumbufu katika miezi mitano ya kwanza ya 2025, kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GAC) zilizotolewa jana Jumatatu, huku jumla ya thamani ya biashara hiyo ikipanda kwa asilimia 2.5 mwaka hadi mwaka, ikitokana na juhudi za nchi hiyo katika kuboresha muundo wake wa biashara na kuimarisha ongezeko la uchumi.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, kiwango hicho kinaongezeka kwa asilimia 0.1 ikilinganishwa na kile kilichorekodiwa katika miezi minne ya kwanza ya 2025 ambapo jumla ya thamani ya biashara ya kuagiza na kuuza bidhaa nje kwa kipimo cha yuan ilifikia yuan trilioni 17.94 (dola za kimarekani kama trilioni 2.5) katika kipindi cha Januari hadi Mei.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya 2025, mauzo ya bidhaa nje ya China yaliongezeka kwa asilimia 7.2 mwaka hadi mwaka kufikia yuan trilioni 10.67 huku uagizaji bidhaa kutoka nje ukishuka kwa asilimia 3.8 hadi kufikia yuan trilioni 7.27.
Picha ikionyesha magari yatakayosafirishwa kuuzwa nje katika Bandari ya Yantai, Mkoa wa Shandong, mashariki mwa China, Januari 2, 2025. (Picha na Tang Ke/Xinhua)
Unyumbufu mkubwa
Lyu Daliang, mkurugenzi wa Idara ya Takwimu na Uchambuzi ya GAC, amesema biashara ya bidhaa ya China imedumisha "unyumbufu mkubwa" licha ya shinikizo kutoka nje, wakati ambapo uchumi wa nchi hiyo ukiendeleza mwelekeo wake wa kuimarika tangu mwanzoni mwa mwaka.
Mwezi Mei pekee, jumla ya biashara ya kuagiza na kuuza nje bidhaa ya China kwa kipimo cha Yuan ilipanda kwa asilimia 2.7 kuliko mwaka jana wakati kama huo. Biashara ya kuuza bidhaa nje iliongezeka kwa asilimia 6.3, huku ile ya kuagiza bidhaa kutoka nje ikishuka kwa asilimia 2.1, kwa mujibu wa takwimu hizo.
Unyumbufu huo umetokana na juhudi za kudhamiria kukuza biashara katika ngazi ya serikali za mitaa.
Picha iliyopigwa Mei 22, 2025 ikionyesha treni ya mizigo ya China-Ulaya X8489 iliyopakiwa magari, vipuri vya mashine na vifaa vya umeme vya matumizi ya nyumbani kabla ya kuondoka kuelekea Duisburg, Ujerumani, mjini Xi'an, Mkoani Shaanxi, kaskazini-magharibi mwa China. (Picha na Sun Jixiang/Xinhua)
Maboresho ya kimuundo
Takwimu hizo za Jumatatu zilizotolewa na GAC pia zinaonyesha maboresho ya kimuundo ya kila mara katika biashara ya nje ya China ambapo mauzo ya bidhaa za teknolojia ya hali ya juu yamefanya vyema katika miezi mitano ya kwanza ya 2025, yakipanda kwa asilimia 6.1 katika kipimo cha dola ya Marekani, huku mauzo ya nje ya bidhaa za mitambo na umeme yakikua kwa asilimia 8.1 katika kipindi hicho.
Kwa upande wa wenzi wa kibiashara, ASEAN imeendelea kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa China katika kipindi cha Januari hadi Mei, ikirekodi jumla ya biashara yenye thamani ya Yuan trilioni 3.02 katika kipindi hicho, ikiongezeka kwa asilimia 9.1 kuliko mwaka jana wakati kama huo.
Katika kipindi hicho, biashara kati ya China na Umoja wa Ulaya ilipanda kwa asilimia 2.9 kufikia yuan karibu trilioni 2.3, wakati biashara yake na Marekani ilipungua kwa asilimia 8.1 kufikia yuan trilioni 1.72, kwa mujibu wa takwimu hizo.
Biashara na nchi washirika wa Ukanda Mmoja, Njia Moja ilipanda kwa asilimia 4.2 kufikia yuan trilioni 9.24, na biashara na nchi za Afrika ilifikia rekodi ya juu, huku kiwango cha biashara kati ya China na Afrika kikiongezeka kwa asilimia 12.4 hadi kufikia yuan bilioni 963.21 katika kipindi hicho.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma